Wanaume katika mkoa wa Shinyanga, wameshauriwa kushiriki kikamilifu katika malezi na makuzi ya watoto, pamoja na kuhakikisha wanapata haki zao za msingi.
| Kaimu Katibu Tawala wa mkoa wa Shinyanga Bw.Samson Hango |
Hango
amewaonya wanaume kutokutumia nafasi zao, nguvu au uwezo wa kiuchumi walio nao kuwadhulumu
na kuwadhalilisha wengine, na badala yake
wavitumie vipawa vyao kujenga familia na jamii yenye misingi ya heshima, utu, upendo
na uwajibikaji.
Amewataka kuwajibika na kuhakikisha watoto wanapata haki zao za msingi ikiwemo matunzo, malezi bora, kulindwa, kupata elimu, huduma za afya na lishe bora na kwamba, wajibu huo unapaswa kuwa endelevu hata pale wanapotengana au kuachana na wenzi wao.
Amewasisitiza
kushirikiana na wenza wao kufuatilia
mienendo ya watoto, mahudhurio yao shuleni, maendeleo yao kitaaluma pamoja na
makundi wanayoshirikiana nayo, ili kubaini mapema na kudhibiti viashiria vya
mmomonyoko wa maadili na mambo mengine yanayowafanya washindwe kuhudhuria
masomo kwa ukamilifu.
Akizungumzia
malezi ya mtoto wa kiume, Hango amebainisha kwamba, maendeleo ya wanaume kwa ujumla wao yanapaswa kwenda pamoja na
wajibu wa kuhakikisha wavulana wanalelewa katika misingi bora, kwa kuwa wao
ndiyo wanaume wa kesho.
Amesema ni
muhimu kuwajenga watoto wa kiume katika misingi ya nidhamu, uadilifu, heshima,
uwajibikaji, uzalendo na kuthamini utu wa kila mtu, pamoja na kuwalinda dhidi
ya ukatili na vitendo vya unyanyasaji wa kingono , ambavyo vinawaweka kwenye
hatari ya kuingiliwa kinyume na maumbile, hali ambayo inachochea vitendo vya
ushoga.
Aidha, amewataka wanaume kuepuka malezi yanayowajengea wavulana dhana kwamba, mwanaume hapaswi kulia, kuomba msaada au kuonyesha hisia zake, badala yake wawafundishe kutambua hisia zao, kuheshimu wengine, kukabiliana na changamoto kwa busara na kuomba msaada kwa wengine pale inapobidi.
Katika hatua
nyingine, Hango amewakumbusha wanaume kutambua wajibu walionao wa kushiriki
kikamilifu katika utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Kupinga Ukatili dhidi ya
Wanawake na Watoto, ili kupunguza vitendo hivyo na hatimaye kuvikomesha kabisa.
Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Mkoa wa Shinyanga, Rehema Edson, amesema jamii ina matarajio makubwa kwa wanaume kutokana na nafasi waliyonayo, hivyo wanapaswa kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto za kifamilia badala ya kuwa chanzo cha migogoro.
| Afisa Maendeleo ya Jamii wa Mkoa wa Shinyanga, Rehema Edson |
Amewaasa
kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao bila kusukumwa, kutumia hekima katika
maamuzi na kuweka mbele maslahi ya familia zao.
Naye Mratibu wa Huduma za Tiba wa Mkoa wa Shinyanga, Joseph Malima, amawakumbusha wanaume umuhimu wa kujali na kulinda afya zao, kwa kuhakikisha wanakwenda kupata huduma za afya na kufanya uchuguzi mara kwa mara, kuchukua tahadhari dhidi ya madhara yanayoweza kujitokeza katika maeneo yao utafuataji, pamoja na kuzingatia ulaji unaofaa.
| Mratibu wa Huduma za Tiba wa Mkoa wa Shinyanga, Joseph Malima |
Wakitoa maoni yao, baadhi ya wanaume walioshiriki maadhimisho hayo wamesema suala la uwajibikaji katika familia halipaswi kuelekezwa kwa wanaume pekee, bali linapaswa kuzingatia pande zote mbili, wanaume na wanawake, ili kujenga familia zenye amani na utulivu.
Wamesema
wanaume wanahitaji kusikilizwa na kushauriwa ndani ya familia badala ya kufokewa, wakieleza kuwa,
mamlaka zinazoshughulikia malalamiko ya migogoro ya kifamilia zinapaswa kutoa
nafasi kwa pande zote kusikilizwa, kabla ya kufanya maamuzi kwa kuangalia hoja
za wanawake pekee.
Kuhusu suala
la malezi wamebainisha kuwa, wakati mwingine linaathiriwa na baadhi ya wanawake
kuwalea watoto kwa upendeleo uliopitiliza na kushindwa kuwawajibisha
wanapofanya makosa au kuonyesha mwenendo usiofaa.
Pia,
wameomba mamlaka za maamuzi kutathmini upya adhabu ya kifungo cha miaka 30 kwa
wanaume na hasa vijana wanaopatikana na hatia ya kuwapa wanafunzi ujauzito,
wakitaka suala hilo liangaliwe kwa kuzingatia mazingira na wajibu wa pande zote
zinazohusika wakiwemo watoto wa kike wenyewe, ambao wamekuwa wakichangia jambo
hilo kwa kuwashawishi kingono watoto wa kiume.
Katika
maadhimisho hayo, washiriki walijadili mada mbalimbali zinazohusu nafasi na
wajibu wa wanaume katika jamii, zikiwemo mwanaume kama kiongozi wa familia,
mwanaume na afya yake, mwanaume na ustawi wa kiuchumi pamoja na ushiriki wa
wanaume katika Mpango wa Taifa wa Bima ya Afya kwa Wote.
Siku ya Kimataifa ya Wanaume huadhimishwa Novemba 19 kila mwaka. Ilianzishwa rasmi mwaka 1999 nchini Trinidad na Tobago kwa lengo la kutambua mchango chanya wa wanaume katika familia na jamii, kuhamasisha afya na ustawi wao, pamoja na kujenga uelewa kuhusu usawa wa kijinsia na umuhimu wa malezi bora.
| Katibu wa mjadala Bw.Frank Nguyu akitangaza maazimio ya yaliyofikiwa |
| Bw. Goodluck Nnko kutoka World Vision mkoa wa Shinyanga akiwasilisha Mada ya Mwanaume na uchumi |
| Mratibu wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanaume Omary Jumanne (mwenye karatasi) akifuatilia maoni ya washiriki |
0 Comments