WASTAAFU SHINYANGA WANUFAIKA NA ELIMU YA MAFAO NA FURSA ZA KIFEDHA ILIYOANDALIWA NA BENKI YA AZANIA

 

Wastaafu kutoka maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Shinyanga, wameipongeza Benki ya AZANIA tawi la Shinyanga, kwa kuwaongezea uelewa kuhusu masuala ya mafao na fursa mbalimbali za kifedha walizonazo, ambazo zinaweza kuwasaidia kuboresha maisha yao.

Wakizungumza baada ya kushiriki semina ya siku moja iliyoandaliwa na benki hiyo, leo Novemba 17, 2026, wamesema elimu waliyoipata imewasaidia kufahamu kwa kina mambo muhimu kuhusu mafao yao, ikiwemo fursa ya kupata mikopo kupitia pensheni zao, hatua ambayo itawasaidia kuinua maisha yao.

Mratibu wa Umoja wa wastaafu Mkoa wa Shinyanga  Bi. Anna Nyagita akitoa Neno la shukrani kwa uongozi wa Benki ya AZANIA kwa niaba ya wenzake

Aidha, wameushukuru uongozi wa juu wa benki hiyo kwa kusikia na kujali ombi lao la kuanzisha tawi katika Manispaa ya Shinyanga, hatua ambayo imewapunguzia usumbufu wa kusafiri umbali mrefu hadi Kagongwa au Kahama kufuata huduma.

Wastaafu hao wametumia nafasi hiyo kuiomba Serikali kupitia mifuko ya hifadhi ya jamii kuendelea kuboresha viwango vya pensheni, ili viendane na hali halisi ya gharama za maisha, ambazo zimeendelea kupanda.

Akizungumza katika semina hiyo, Meneja wa Benki ya AZANIA Tawi la Shinyanga, Kiyenze Nsomi, amewaomba wastaafu kuendelea kuiamini benki hiyo, akieleza kuwa ni miongoni mwa benki zinazoongoza nchini kwa uwekezaji, jambo linaloiwezesha kutoa huduma bora na za uhakika kwa wateja wake.

Meneja wa Benki ya AZANIA Tawi la Shinyanga, Kiyenze Nsomi akizungumza na wastaafu

Amesema benki hiyo imeweka utaratibu wa kutoa huduma za kifedha zinazozingatia mahitaji ya makundi mbalimbali ya kijamii, yakiwemo ya wastaafu, ambao wanaweza kunufaika na mikopo yenye masharti nafuu kwa kutumia pensheni zao, kupitia makubaliano na taasisi zinazowalipa.

Kwa upande wake, Afisa Mahusiano wa Benki ya AZANIA Tawi la Shinyanga, Novatus Grevase, amesema benki hiyo imeboresha mifumo ya utoaji mikopo kwa wastaafu ili kurahisisha upatikanaji wa huduma, ambapo imewaondolea usumbufu wa kutembea huku na kule kutafuta nyaraka nyingi kutoka katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).

Afisa Mahusiano wa Benki ya AZANIA Tawi la Shinyanga, Novatus Grevase
 akizungumza na wastaafu kwenye Semina

Amesema kupitia mfumo maalumu unaoiunganisha benki hiyo na PSSSF, taratibu nyingi za mikopo hufanyika ndani ya benki, hivyo kuwawezesha wastaafu kupata huduma kwa urahisi zaidi.

Aidha, amesema benki hiyo ina utaratibu wa kutoa mikopo hata kwa wastaafu wenye umri wa zaidi ya miaka 80, tofauti na baadhi ya benki ambazo huweka ukomo wa umri wa chini zaidi katika utoaji wa mikopo.

Naye Afisa Matekelezo Mwandamizi wa PSSSF mkoa wa Shinyanga, Gwamaka Ngomale, amesema mfuko huo unaendelea kuboresha mafao ya wastaafu, akibainisha kuwa, hatua mojawapo iliyochukuliwa ni kuongeza kiwango cha chini cha pensheni kutoka Shilingi Laki moja hadi Shilingi 250 Elfu.

Afisa Matekelezo Mwandamizi wa PSSSF mkoa wa Shinyanga Gwamaka Ngomale

Amewataka wastaafu na watumishi wanaokaribia kustaafu kuhakikisha wanakamilisha nyaraka zote zinazohitajika wakati wa kuwasilisha madai ya mafao yao.

Pia amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha ndoa zao zinasajiliwa na kutambulika kisheria, ili kuwawezesha wenzi wao kupata mafao wanayostahili endapo mwanachama atafariki dunia, bila kukumbana na changamoto za kiutawala na kisheria.

Aidha, aliwahimiza wastaafu wanaokumbana na changamoto katika mchakato wa kupata mafao yao kufika katika ofisi za PSSSF, kwa ajili ya kupata msaada wa kutatua changamoto zao.

Kupitia semina hiyo ambayo imefanyika kwenye Bwalo la Jeshi, Kambarage katika Manispaa ya Shinyanga, wastaafu pia wamepata elimu kutoka kwa maafisa wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa watumishi wa Sekta binafsi (NSSF), walioeleza kuhusu utaratibu wa mafao kwa watumishi wa Sekta binafsi, fursa zilizopo na namna ya kujiunga na mfuko huo kupitia Skimu ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii, kwa wananchi wanaofanya kazi katika sekta isiyo rasmi.

Vilevile, maafisa wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) walitoa elimu kuhusu masuala mbalimbali ya bima ya afya, ikiwemo mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, huku afisa kutoka Hazina Ndogo akitoa ufafanuzi kuhusu masuala yanayohusu mafao ya wastaafu.

Benki ya Azania imeendelea kutoa huduma za kifedha katika maeneo mbalimbali nchini, huku ikiweka mkazo katika kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia mikopo maalumu yenye masharti nafuu na inayozingatia mahitaji ya makundi mbalimbali ya kijamii.

Makundi hayo ni pamoja na wastaafu, wanawake, wakulima, wafanyabiashara, vikundi vya wajasiriamali, watumishi wa sekta binafsi na watu binafsi.

Afisa Mafao wa NSSF mkoa wa Shinyanga Mokwe Kisigiro akitoa elimu kwa wastaafu
Afisa matekelezo wa NSSF Mkoa wa Shinyanga Janeth Katemi akitoa elimu kwa wastaafu
Mwakilishi wa NHIF Mkoa wa Shinyanga akitoa elimu kwa wastaafu
Afisa Hazina ndogo mkoa wa Shinyanga Mary Mpangala akitoa elimu kwa wastaafu 
Mwenyekiti wa umoja wa wastaafu mkoa wa Shinyanga Nsolo Stephen akizungumza kwa niaba ya wastaafu wote

Post a Comment

0 Comments