Benki ya AZANIA, Tawi la Shinyanga, inatarajia kuendesha semina maalumu kwa wastaafu zaidi ya 300, ikiwa na lengo la kuwajengea uwezo kuhusu usimamizi na matumizi bora ya fedha, pamoja na kuwafahamisha huduma mbalimbali za kibenki zinazotolewa na benki hiyo.
Semina hiyo ambayo itaanza saa 2:00 asubuhi, inatarajiwa
kufanyika kesho Jumanne tarehe 17, Novemba 2026, katika Bwalo la Jeshi,
Kambarage mjini Shinyanga, na itawakutanisha wastaafu kutoka maeneo mbalimbali
ya Wilaya ya Shinyanga.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya semina hiyo, Afisa Mahusiano wa Benki ya AZANIA, Tawi la Shinyanga, Novatus Grevase, amesema washiriki watapata elimu kuhusu huduma za kibenki zinazotolewa na benki hiyo, hususan mikopo na namna bora ya kusimamia na kutumia fedha wanazopata.
![]() |
| Afisa Mahusiano wa Benki ya AZANIA, Tawi la Shinyanga, Novatus Grevase |
Aidha,
amesema semina hiyo itashirikisha taasisi mbalimbali ambazo ni wanahisa wa
Benki hiyo, ambao ni pamoja na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma
(PSSSF), Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa watumishi wa Sekta binafsi (NSSF) na Mfuko
wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
Wadau hao
kwa pamoja watatoa elimu juu ya huduma mbalimbali wanazozitoa ,hususan
zinazowalenga wastaafu.
Benki ya
AZANIA ambayo inatoa huduma za kifedha katika maeneo mbalimbali nchini,
imeendelea kuweka mkazo katika suala la kuwainua wananchi kiuchumi, kwa kutoa
mikopo maalumu yenye riba nafuu na masharti yanayozingatia mahitaji ya makundi
mbalimbali ya kijamii.
Makundi hayo ni pamoja na wastaafu, wanawake, wakulima, wafanyabiashara, vikundi vya wajasiriamali, watumishi wa sekta binafsi na watu binafsi.



0 Comments