Daraja la
Minzi, linalowaunganisha wakazi wa mitaa ya Mbuyuni na Dome, Kata za Ndembezi katika
Manispaa ya Shinyanga, linatarajiwa kujengwa upya, ili liweze kukidhi mahitaji
ya watumiaji.
Akizungumza
na wananchi wa Mtaa wa Dome kwenye mkutano wa hadhara kwa lengo la kuwashukuru kwa kumchagua yeye na viongozi wengine chama cha mapinduzi (CCM), Diwani wa kata ya Ndembezi, Pendo Sawa, amesema
mchakato wa ujenzi wa daraja hilo tayari umeanza baada ya hoja hiyo kupitishwa
na Baraza la Madiwani la Manispaa ya Shinyanga, ambapo utekelezaji wa mradi huo
utafanyika ndani ya mwaka huu wa fedha 2026/2027.
Amesema
ujenzi wa daraja hilo unatarajiwa kugharimu takribani Shilingi milioni 123 mpaka kukamilika kwake, ambapo
litawaondolea wananchi adha ya kufurika kwa maji kwenye eneo hilo hasa mvua
zinaponyesha, hali inayowaletea usumbufu.
Katika hatua
nyingine, Sawa amesema anaendelea kushirikiana na viongozi wengine, akiwemo
Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Paschal Patrobas Katambi, katika
kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili wananchi wa Kata ya Ndembezi.
Ametaja
baadhi ya changamoto zilizotafutiwa ufumbuzi kuwa ni pamoja ujenzi wa Daraja la
Butengwa, kufungua barabara za mitaa kwenye maeneo ya makazi mapya, kujenga
mifereji ya maji pamoja na kushughulikia mgogoro wa ardhi kati ya wananchi wa
mtaa wa Butengwa na kampuni ya CASEC ambao tayari umetatuliwa.
Sawa pia ameeleza kuhusu mchakato unaoendelea wa kuwarejesha wafanyabiashara wa Milunda kutoka Matanda kwenda eneo la Dome Garden, Kata ya Ndembezi, hatua ambayo ameitaja, inalenga kufungua na kuongeza fursa za kiuchumi na kibiashara kwa wananchi wa eneo hilo.
0 Comments