Ziara za kushtukiza zilizokuwa zikifanywa na viongozi wa Serikali katika miaka ya nyuma, zilisaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha utendaji na uwajibikaji wa watumishi wa umma, jambo lililochangia kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Utaratibu
huo uliwafanya watendaji wa taasisi za umma kuwa tayari wakati wote, kwa kuwa
hawakujua siku wala saa ambayo kiongozi angefika kukagua utekelezaji wa
majukumu yao. Hali hiyo ilisaidia kupunguza uzembe na kufanya kazi kwa mazoea,
kwani kila mtendaji alilazimika kuwajibika ipasavyo ili kuepuka kubainika kwa
mapungufu aliyonayo na kuchukuliwa hatua.
Hata hivyo,
kutokuwepo kwa ziara hizo kumechangia baadhi ya watendaji wazembe kurejea
katika utendaji wa mazoea, hali inayoweza kuathiri ufanisi na ubora wa huduma
zinazotolewa kwa wananchi.
Kwa msingi
huo, viongozi wa Serikali wanapaswa kuendeleza utaratibu wa kufanya ziara za
kushtukiza ili kuongeza uwajibikaji na kuboresha utendaji. Hata hivyo, ziara
hizo hazipaswi kufanywa kwa lengo la kumdhalilisha au kumkomesha mtumishi,
kumvunja moyo au kumtia hofu, bali zifanyike kwa weledi, hekima na busara.
Viongozi
wanapaswa kutumia ziara hizo kubaini changamoto zinazowakabili watendaji,
kusikiliza maoni yao na kutoa miongozo ya kuboresha utendaji kabla ya kuchukua
hatua pale inapobainika kuna uzembe au ukiukwaji wa taratibu.
Aidha, ziara hizo zinapaswa kufanyika kwa usiri ili ziendelee kuwa na maana na kuleta matokeo chanya, badala ya kutumika kama njia ya kutafuta umaarufu au kujijenga kwa kiongozi mmoja. Lengo kuu linapaswa kuwa kuimarisha uwajibikaji, kuongeza ufanisi na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.

0 Comments