WANANCHI DOME WAMUOMBA MWENYEKITI KUENDELEA KUPIGANIA MIRADI YA MAENDELEO

Wananchi wa Mtaa wa Dome, Kata ya Ndembezi katika Manispaa ya Shinyanga, wamemuomba Mwenyekiti wa mtaa huo, Solomon Nalinga Najulwa, kuendelea kupigania miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya barabara.

Rai hiyo imetolewa na wananchi hao katika Mkutano wa Hadhara ulioitishwa na Mwenyekiti huyo, kwa ajili ya kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za mtaa kwa kipindi cha robo mwaka, kuanzia mwezi Mei hadi Julai, 2026.

Wananchi hao wamempongeza Mwenyekiti huyo kwa juhudi anazofanya katika kushughulikia changamoto mbalimbali kwenye mtaa wao, ikiwemo kuimarisha ulinzi na usalama, pamoja na kuchochea shughuli za maendeleo katika mtaa huo.

Wamesema juhudi hizo zimewezesha kaya zote zisizokuwa na uwezo ambazo ni walengwa wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kunufaika na bima ya afya kwa wote, huku wazee 48 wanaoishi katika mtaa huo wakipata msamaha wa gharama za matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.

Pamoja na kueleza kuridhishwa na juhudi za Mwenyekiti huyo katika kupigania na kusimamia maslahi yao, wamemuomba aendelee kutoa msukumo kwa mamlaka ili changamoto za miundombinu ya barabara, hasa katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa, ziweze kutatuliwa.

Katika taarifa yake ya robo mwaka, Najulwa amebainisha kuwa, Ofisi ya Mtaa imefanikiwa kushughulikia masuala mbalimbali ikiwemo kutatua migogoro midogomidogo 28 ya kijamii, hatua ambayo imesaidia kurejesha mahusiano mema na kudumisha hali ya amani katika mtaa huo.

Amesema shughuli nyingine zilizofanyika ni pamoja na kufuatilia uboreshaji wa miundombinu ya barabara, kusaidia vikundi mbalimbali kupata mikopo inayotolewa na Halmashauri, pamoja na kuwatambulisha vijana pale zinapotokea fursa za ajira.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali ya Mtaa na kushiriki kikamilifu katika masuala ya ulinzi na usalama ili kudumisha amani.

Pia amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika shughuli za Mwenge wa Uhuru, ambao unatarajiwa kupokelewa katika Manispaa ya Shinyanga Agosti 19, 2026.

Naye Diwani wa Kata ya Ndembezi, Pendo John Sawa ambaye alihudhuria Mkutano huo, amempongeza Mwenyekiti huyo pamoja na wajumbe wa Serikali ya Mtaa kwa juhudi zao za kushughulikia na kutatua migogoro midogomidogo.

Sawa ambaye pia ni Naibu Meya wa Manispaa ya Shinyanga, amesema hatua hiyo imeiwezesha Ofisi ya Kata kupata nafasi ya kutosha kushughulikia miradi ya maendeleo, badala ya kutumia muda mwingi kushughulikia migogoro.

Mkutano huo wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Bustani ya Dome (Dome Garden), na kuhudhuriwa na Diwani wa Kata ya Ndembezi Pendo Sawa, pia ulihudhuriwa na Afisa Mtendaji wa Kata ya Ndembezi, Adella Mukinga.


Afisa Mtendaji wa Kata ya Ndembezi, Adella Mukinga. akizungumza na wananchi wa Mtaa wa Dome


Diwani wa Kata ya Ndembezi, Pendo John Sawa akizungumza na wananchi wa mtaa wa Dome kwenye mkutano



 

Post a Comment

0 Comments