MAMLAKA ZIKOMESHE UTAPELI HUU

Kumekuwa na ongezeko la malalamiko kuhusu makundi yanayodaiwa kujiendesha kama kampuni na kutumia matangazo ya ajira kuwavutia wananchi, hasa vijana, kwa ahadi za ajira zenye mishahara mizuri, nafasi za usimamizi wa biashara na fursa nyingine za kiuchumi.

Pamoja na jambo hilo kuwa la muda mrefu, hivi karibuni matukio hayo yameripotiwa kutokea kwa kufuatana katika mikoa mbalimbali ikiwemo Mbeya, Pwani, Iringa na Manyara.

Kinachotia wasiwasi ni kwamba, baadhi ya nafasi hizo hutangazwa bila kuweka wazi vigezo vya msingi vya ajira, huku waombaji wakiahidiwa kuajiriwa au kupewa nafasi za kusimamia biashara ambazo wakati mwingine hakuna uthibitisho wa kutosha kuhusu kampuni au shughuli hizo.

Baada ya kuvutiwa na matangazo hayo, waombaji huitwa katika ofisi ambazo mara nyingi ziko kwenye maeneo yaliyofichika. 

Baadhi yao wanapofika hukuta mazingira tofauti na matarajio yao, yakiwemo makundi ya vijana wenzao wanaoishi pamoja katika mazingira yasiyofaa kiafya na kiusalama, huku wakiendelea kuahidiwa kwamba taratibu za ajira zinaendelea.

Kadiri siku zinavyokwenda, baadhi yao huanza kuombwa fedha kwa ajili ya chakula, malazi, usajili, vitambulisho, mafunzo na vifaa vya kazi. Wengine hutakiwa kununua vifaa vya gharama kubwa, ikiwemo kompyuta mpakato, kwa maelezo kwamba ni sehemu ya maandalizi kabla ya kuajiriwa.

Baadhi ya vijana waliowahi kuingia kwenye mtego huo,  wanadai kuzuiwa hata kuwasiliana kwa uhuru na ndugu zao au watu wengine wa nje, lakini wakati huohuo hulazimishwa kuwapigia simu wazazi na ndugu zao wakiwa chini ya uangalizi, ili kuwaomba fedha au kuwashawishi watu wengine kujiunga na mpango huo.

Jambo hili linaweza kuwaumiza si vijana pekee, bali pia familia zao. Baadhi ya wazazi, kwa kutarajia watoto wao kupata ajira, hulazimika kutumia akiba au kuuza mali ili kupata fedha zinazohitajika. Mwisho wa siku, iwapo ahadi ya ajira haitimizwi, familia hizo huachwa katika hasara kubwa.

Ripoti za matukio ya aina hii zimekuwa zikijitokeza katika maeneo mbalimbali nchini, jambo linaloonyesha umuhimu wa mamlaka husika kulifuatilia kwa karibu na kuchukua hatua stahiki pale sheria zinapokiukwa.

Ni wakati sasa kwa mamlaka zinazohusika na ajira, biashara, ulinzi na usalama kushirikiana kufuatilia makundi na kampuni zinazotoa matangazo ya ajira yanayotia shaka. 

Aidha, wananchi wanapaswa kuendelea kupewa elimu kuhusu taratibu halali za kutafuta ajira na viashiria vya utapeli ili wasipoteze fedha, muda na mali zao.

Kukosekana kwa hatua madhubuti dhidi ya vitendo hivi kunatoa nafasi kwa waathirika kuongezeka. Mamlaka zisisubiri malalamiko yaongezeke au madhara kuwa makubwa,  zinapaswa kuchukua hatua mapema ili kulinda vijana, familia zao na heshima ya soko la ajira nchini.

 

Post a Comment

0 Comments