MWENGE WA UHURU KUPOKELEWA KATIKA MANISPAA YA SHINYANGA AGOSTI 19, 2026


Wananchi wa Manispaa ya Shinyanga wameombwa kujitokeza kwa wingi kushiriki mapokezi ya Mwenge wa Uhuru, unaotarajiwa kuwasili katika manispaa hiyo Jumatano, Agosti 19, 2026, ukitokea Wilaya ya Kishapu.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Dkt. Alexius Kagunze, Mwenge wa Uhuru utapokelewa katika eneo la Kolandoto majira ya saa 1:30 asubuhi, kabla ya kuendelea na shughuli mbalimbali za kutembelea, kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo.

Miradi inayotarajiwa kuzinduliwa ni pamoja na mradi wa upanuzi wa mtandao wa maji katika Kata ya Kolandoto, Zahanati ya Kijiji cha Mwagala iliyopo Kata ya Ibadakuli, mradi wa duka la nishati mbadala ya kupikia wa kikundi cha Wanawake na Samia kilichopo Kata ya Ndembezi, pamoja na Daraja la Dodoma.

Aidha, Mwenge huo utazindua madarasa manne katika Shule ya Sekondari Old Shinyanga, kuweka jiwe la msingi katika mradi wa mwekezaji binafsi wa Makindo Royal Hotel 
pamoja na kuzindua Klabu ya wapinga rushwa katika Shule ya Sekondari Old Shinyanga.

Shughuli nyingine zitakazotembelewa ni pamoja na kukagua shughuli za kikundi cha vijana cha Mkasa Fashion kilichopo Kata ya mjini, kinachonufaika na mkopo ambao ni sehemu ya asilimia 10 inayotolewa kwa makundi mbalimbali kutokana na mapato ya ndani Halmashauri.

Baada ya kukamilisha shughuli za kutembelea, kukagua na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo, Mwenge wa Uhuru utakesha katika Uwanja wa Sabasaba mjini Shinyanga.

Mkesha huo utaambatana na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali wa ndani na nje ya Manispaa ya Shinyanga.

Mwenge huo utakabidhiwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga (vijijini) siku ya Alhamisi, Agosti 20, 2026 kwa ajili ya kuendelea na mbio zake katika Halmashauri hiyo.
 

Post a Comment

0 Comments