Ukifuatilia kwa undani, changamoto hii haiwezi kuhusishwa
na Serikali au taasisi nzima, bali mara nyingi husababishwa na udhaifu katika
usimamizi na uwajibikaji wa baadhi ya watendaji.
Wapo baadhi ya viongozi na wasimamizi ambao hawafuatilii
kwa karibu namna watumishi walio chini yao wanavyotekeleza majukumu na
kuwahudumia wananchi.
Ni muhimu kwa viongozi wa taasisi kujenga utamaduni wa kutembelea maeneo ya kutolea huduma, kuzungumza moja kwa moja na wananchi na kusikiliza maoni yao.
Ufuatiliaji wa aina hiyo unaweza kusaidia kubaini mapema
uzembe, ucheleweshaji usio wa lazima na vitendo vinavyoweza kuwafanya wananchi
kuamini kuwa ili kupata huduma ni lazima watoe kitu.
Si jambo la kawaida kwa mwananchi kusafiri kutoka kijijini
au eneo la mbali kwa ajili ya kupata huduma ambayo, kiuhalisia, inaweza
kukamilishwa ndani ya siku moja, lakini akafika katika ofisi husika na kuambiwa
arudi siku nyingine bila sababu ya msingi. Hali hiyo si tu kwamba inampotezea
muda na kumwongezea gharama, bali pia inaweza kumjengea mtazamo hasi kuhusu
huduma za Serikali.
Kwa hiyo, viongozi na wasimamizi wa taasisi za umma wanapaswa kuimarisha ufuatiliaji wa utendaji wa watumishi walio chini yao na kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa wakati, kwa haki na kwa heshima huku wale wanaobainika kuwa kikwazo kwa ufanisi wa taasisi waondolewe mara moja au wapangiwe majukumu mengine.
Wananchi wanapopata huduma bora, malalamiko hupungua, imani kwa taasisi
huongezeka na taswira ya Serikali huimarika.
Ni muhimu kutambua kuwa, mara nyingi, kasoro za watumishi wachache zinaweza kuwafanya wananchi kuichukulia Serikali nzima kuwa haiwajali. Hivyo, uongozi madhubuti, ufuatiliaji wa karibu na uwajibikaji wa watendaji ni sehemu muhimu ya kuhakikisha huduma za umma zinatolewa kwa ufanisi na si kwa matashi ya mtu kwa sababu tu yuko kwenye nafasi hiyo.

0 Comments