Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Azza Hillal Hamad, amesema barabara ya kutoka Njia panda ya Luhumbo hadi Didia yenye urefu wa kilomita 4.5 inatarajiwa kujengwa kwa kiwango cha lami, hatua itakayorahisisha usafiri na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa eneo hilo.
Azza ameyasema hayo , wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Didia katika mkutano wa hadhara wa
kusikiliza kero zao na kutoa mrejesho wa utekelezaji wa ahadi mbalimbali za
maendeleo.
Amesema ujenzi wa barabara hiyo ulikuwa kati ya maombi
makubwa yaliyotolewa na wananchi wakati wa kampeni za uchaguzi, na kwamba
tayari suala hilo limewasilishwa bungeni huku Wakala wa Barabara Mijini na vijijini (TARURA) Mkoa wa Shinyanga akiwa amekamilisha tathmini na kuwasilisha
taarifa TAMISEMI kwa hatua zaidi.
"Changamoto ya barabara ya kutoka Njia panda ya
Luhumbo hadi Didia Center inaelekea kupata ufumbuzi kwa kujengwa kwa kiwango
cha lami," amesema Azza.
Akizungumzia maendeleo mengine yanayotekelezwa na Serikali
ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Ilani ya CCM, Azza amesema ndani ya
kipindi kifupi baada ya kuanza kutekelezwa kwa ilani hiyo, fedha mbalimbali
zimetolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika eneo hilo.
Amesema Shule ya Sekondari Luhumbo imepokea shilingi
milioni 113 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa manne, huku Shule ya Msingi Didia
ikipokea shilingi milioni 105 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa manne pamoja na
ununuzi wa madawati.
Aidha, amesema majengo ya zamani ya Shule ya Msingi Didia
yamechakaa kiasi kwamba yanahitaji kujengwa upya badala ya kufanyiwa ukarabati.
"Shule hii ni ya muda mrefu na majengo
yake yamechakaa. Serikali imesikia kilio cha wananchi na tayari fedha
zimepatikana. Si muda mrefu tutaanza kuona shule yetu ikiwa katika mazingira
bora zaidi," amesema.
Katika sekta nyingine, Azza amesema Serikali imetoa
shilingi milioni 56 kwa ajili ya ujenzi wa machinjio ya kisasa katika Kijiji
cha Didia, pamoja na shilingi milioni 438 kwa ajili ya ujenzi wa mita 300 za
mitaro katika Mji Mdogo wa Didia.
Pia amesema shilingi milioni 69 zimetolewa kwa ajili ya
ujenzi wa barabara za ndani na makalavati, huku shilingi milioni 16
zikielekezwa kujenga matundu 23 ya vyoo katika Shule ya Msingi Didia.
Kwa upande wa uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, amesema
vikundi vitatu vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika Mji Mdogo wa
Didia vimepokea mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 56.9.
Azza pia amesema ameendelea kuishawishi Serikali kujenga
Kituo cha Afya Didia ili kusogeza huduma za matibabu karibu na wananchi,
akieleza kuwa ombi hilo limewasilishwa katika bajeti ya mwaka huu wa fedha.
Katika mkutano huo, wananchi wamewasilisha kero mbalimbali
zikiwemo ukosefu wa stendi ya mabasi, upatikanaji wa huduma ya umeme katika
baadhi ya vitongoji na changamoto nyingine za miundombinu, huku Mbunge huyo
akiahidi kuendelea kuzifuatilia kwa kushirikiana na Serikali hadi zipatiwe
ufumbuzi.
Mji wa Didia, uliopo katika Jimbo la Itwangi, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga (Vijijini), unasifika kwa shughuli za biashara ya mazao ya kilimo, hususan mpunga na mchele.
Aidha, eneo hilo lina taasisi kubwa za elimu, ikiwemo Shule ya Sekondari Don Bosco, inayomilikiwa na Mapadre Wasalesiani wa Shirika la Mtakatifu Don Bosco na inayotambulika kwa kukuza vipaji pamoja na kutoa elimu bora nchini.






0 Comments