Msimu wa
mvua za Vuli wa mwaka 2026, unaotarajiwa kuanza Oktoba hadi Desemba,
unatarajiwa kuwa na mvua za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo
mbalimbali yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya hewa Tanzania(TMA) mvua hizo zinatarajiwa kuwa na hali ya El Niño yenye nguvu, huku maeneo ya Ukanda wa Pwani ya Kaskazini, Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, Ukanda wa Ziwa Viktoria pamoja na kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma yakitarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.
Mvua hizo zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya nne ya Septemba na wiki ya kwanza ya Oktoba 2026, katika maeneo ya Ukanda wa Ziwa Viktoria, kabla ya kusambaa taratibu katika maeneo mengine mwezi Oktoba.
TMA imetahadharisha kuwa, mvua hizo zinaweza kusababisha mafuriko katika baadhi ya maeneo, hali inayoweza kuathiri ukuaji wa mazao na miundombinu ya kilimo.
Pia, ongezeko la kina cha maji katika mito na mabwawa linatarajiwa, jambo linaloweza kuathiri miundombinu ya maji na nishati, pamoja na kuongeza hatari ya kutokea kwa magonjwa ya mlipuko.
Kutokana na mwelekeo huo, wadau katika sekta za kilimo na usalama wa chakula, mifugo na uvuvi, utalii na wanyamapori, usafiri, nishati, ujenzi, maji na madini, afya pamoja na menejimenti za maafa wanashauriwa kuchukua tahadhari na kujiandaa mapema ili kupunguza athari zinazoweza kujitokea.
SOURCE TMA

0 Comments