NSSF SHINYANGA YABAINISHA FAIDA ZA KUJIUNGA NA HIFADHI SKIMU


Mfuko wa hifadhi ya jamii (NSSF) mkoa wa Shinyanga,
 umewashauri wananchi kuchangamkia fursa ya kujiunga na huduma ya Skimu ya taifa ya hifadhi jamii kwa sekta isiyo rasmi, ambayo inawalenga wanachama waliojiajiri.

Meneja wa NSSF mkoa wa Shinyanga Bi.Amina Mdabi ameiambia Shinyanga One Media kuwa, fursa hiyo imekuja kufuatia mabadiliko ya sheria ya hifadhi ya jamii, yaliyotoa nafasi kwa watu waliojiajiri wenyewe kutoka kwenye sekta isiyo rasmi kuwa wanachama wa NSSF, na kunufaika na mafao mbalimbali kama ilivyo kwa wale walioajiriwa kwenye Sekta binafsi.

Amesema sheria hiyo imeanza kutumika rasmi mwanzoni mwa mwaka huu 2026, ambapo kwa sasa watu waliojiajiri wenyewe kupitia sekta isiyo rasmi ikiwemo kilimo, ufugaji, uvuvi, uchimbaji mdogo wa madini, kazi za Sanaa, Bodaboda, Mama lishe, Wamachinga,  na biashara nyingine ndogondogo wanaruhusiwa kuwa wanachama wa NSSF na kunufaika na mafao mbalimbali.

Bi. Mdabi ameyataja mafao watakayonufaika nayo kuwa ni pamoja na matibabu, ambapo fao hilo hutolewa kwa familia isiyozidi watu sita, likijumuisha mwanachama mwenyewe, mwenza wake na watoto wao wasiozidi wanne,  na kwamba, watapata huduma za afya kuanzia Hospitali za kawaida mpaka za rufaa kulingana na miongozio iliyowekwa

Mafao mengine ni Pensheni ya uzee, mafao ya urithi, mafao ya ulemavu, mafao ya uzazi kwa wanawake na mafao ya msaada wa mazishi.

Akifafanua kuhusu fao la matibabu amesema, kwa sasa NSSF inapokea wanachama  wenye uwezo wa kuchangia kiasi cha kuanzia Shilingi Elfu Thelathini kwa mwezi na kuendelea, ambapo mwananchama anayechangia kuanzia Shilingi elfu Thelathini pekee atapata fao la matibabu yeye peke yake na yule anayechangia kuanzia shilingi Elfu Hamsini na mbili na miambili atapata fao la matibabu yeye, mwenza wake na watoto wasiopungua wanne.

Amebainisha kwamba, huduma ya matibabu inaanza kutolewa baada tu ya miezi mitatu ya uchangiaji.

Meneja huyo wa NSSF, amewaomba wananchi kuchangamkia fursa hiyo na kujitokeza kwa wingi kujiunga na Hifadhi skimu, na kwamba maelezo zaidi ya namna ya kujiunga watayapata kwa kutembelea Ofisi za NSSF zilizopo karibu yao au kwenye mifumo rasmi ya taarifa ya NSSF.

Jengo la NSSF mkoa wa Shinyanga

Skimu ya taifa ya hifadhi jamii kwa Sekta isiyo rasmi, ilianzishwa kwa lengo la kuungana mkono  juhudi za Serikali za kupunguza umaskini kwa wananchi, kuchochea uchumi na kuchochea kasi ya maendeleo.


 

 

 

Post a Comment

0 Comments