WANANCHI KISESA WAFUNGA BARABARA BAADA YA MWANAFUNZI KUGONGWA GARI

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mtafungwa

Jeshi la Polisi limelazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya baadhi ya wananchi katika eneo la Kisesa, Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, baada ya wananchi hao kufunga barabara kuu ya Mwanza–Musoma kufuatia tukio la mwanafunzi wa darasa la kwanza, Prosper Msafiri (7), aliyegongwa na lori na kufariki dunia.

Tukio hilo limetokea leo, Agosti 13, 2026, majira ya saa 11:45 asubuhi katika Kijiji na Kata ya Kisesa, Tarafa ya Sanjo, Wilaya ya Magu.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mtafungwa, mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Wita na mkazi wa Kisesa, alikuwa akivuka barabara kutoka upande wa kulia kwenda kushoto alipogongwa na lori hilo.

Kamanda Mtafungwa amesema lori lililohusika katika ajali hiyo ni lenye namba za usajili T 885 ENK, aina ya Scania, mali ya Kampuni ya Seedco Tanzania Limited, lililokuwa likisafiri kutoka Mwanza mjini kuelekea Bariadi.

Amesema lori hilo lilikuwa likiendeshwa na Mdamo Nyalwisila (40), mkazi wa Bariadi, ambaye tayari amekamatwa na anashikiliwa na Polisi kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.

Kamanda Mtafungwa amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa ajali hiyo ilisababishwa na uzembe wa dereva kushindwa kuchukua tahadhari alipokuwa akiendesha katika eneo lenye makazi ya watu.

Kufuatia kifo hicho, wananchi waliokuwa eneo la tukio walifunga barabara kuu ya Mwanza–Musoma na kuzuia magari kupita, wakitaka hatua zichukuliwe dhidi ya dereva pamoja na kuwekwa hatua za kudhibiti mwendo wa magari katika eneo hilo.

Viongozi mbalimbali wa Serikali walifika eneo la tukio na kufanya mazungumzo na wananchi, huku wakiwaomba kuwa watulivu na kuacha vyombo vya dola vichukue hatua kwa mujibu wa sheria.

Aidha, ombi la wananchi la kuwekwa matuta katika eneo hilo lilikubaliwa, hatua inayolenga kupunguza mwendo wa magari na kuongeza usalama kwa wakazi pamoja na watumiaji wengine wa barabara.

Hata hivyo, licha ya wito huo, baadhi ya wananchi walikaidi na kuanza kurusha mawe, hali iliyosababisha Polisi kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya na kurejesha utulivu.

Kamanda Mtafungwa amewataka madereva kuwa makini na kuzingatia taratibu za usalama wanapopita katika maeneo yenye makazi ya watu, ikiwemo kupunguza mwendo na kufuata alama za barabarani.

Pia amewataka watembea kwa miguu na watumiaji wengine wa barabara kuchukua tahadhari wanapovuka au kutumia barabara, huku wazazi wakihimizwa kuwafuatilia na kuwaongoza watoto wadogo ili kuepusha ajali zinazoweza kuzuilika.

(Chanzo IPP Media)

  

Post a Comment

0 Comments