SIDO SHINYANGA YAWAHIMIZA WANANCHI KUCHANGAMKIA FURSA INAZOZITOA

Kaimu Meneja wa SIDO Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Ally Mtwale

Shirika la kuendeleza Viwanda Vidogo (SIDO) Mkoa wa Shinyanga, limeendelea kuwawezesha wananchi, wakiwemo wafanyabiashara na wajasiriamali, kupitia huduma mbalimbali zinazolenga kuongeza uzalishaji na kukuza fursa za kiuchumi.

Kaimu Meneja wa SIDO Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Ally Mtwale, amesema shirika hilo limekuwa likiwajengea uwezo wananchi kupitia mafunzo ya uendelezaji wa biashara, kuongeza thamani ya bidhaa zao, mikopo yenye masharti nafuu, huduma za masoko pamoja na utengenezaji wa mashine za kuongeza thamani na kuendeleza mazao ya kilimo.

SIDO Shinyanga, pia inatengeneza vifaa vya uchenjuaji wa madini na vifaa vya ujenzi.

Amesema wana mitambo ya kisasa ya kutengeneza mashine mbalimbali zinazouzwa kwa gharama nafuu, ikiwa ni sehemu ya kuwawezesha wananchi kuongeza thamani ya bidhaa wanazozalisha na kuongeza mapato, pamoja na kuendeleza viwanda vidogo na vya kati.

Ametaja baadhi ya mashine zinazotengenezwa na SIDO mkoa wa Shinyanga  kuwa ni za kupukuchua mahindi, kusaga na kukoboa nafaka, kubangua na kukaanga karanga, kusindika ngozi, kuzalisha bidhaa za ngozi kama vile mikanda na viatu na mashine za kuchakata Katani na migomba kwa lengo la kupata nyuzi zinazotumika kuzalisha bidhaa mbalimbali ikiwemo kamba, mazulia na vikapu.

Mhandisi Mtwale amesema mashine hizo ni imara na zinapatikana kwa gharama nafuu, huku akibainisha kuwa, lengo la SIDO siyo kufanya biashara na badala yake ipo kwa ajili ya kukuza viwanda, kuendeleza biashara na kuongeza ajira, ili kusaidia mpango wa Serikali wa kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi na kuboresha maisha yao.

Kuhusu huduma za kifedha, amesema SIDO inatoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wajasiriamali, kuanzia Shilingi 100,000 hadi milioni 6.5, ambapo kwa wale wenye vigezo wanaohitaji mikopo mikubwa, SIDO hutoa dhamanama kwenye benki walizoingia nazo ubia za  Azania na CRDB.

Kuhusu masoko, amesema SIDO hutoa mafunzo ya masoko na kuandaa maonesho mbalimbali yanayowapa wafanyabiashara na wajasiriamali fursa ya kubadilishana uzoefu, kuongeza wateja na kutangaza bidhaa zao kwa wateja wa ndani na nje ya nchi.

Amesema maonesho hayo kitaifa kwa mwaka huu, yatafanyika mkoani Shinyanga kwenye uwanja wa Magufuli katika Manispaa ya Kahama, kuanzia Oktoba 21 hadi 30, 2026, ambapo amewahimiza  wafanyabiashara na wajasiriamali kutumia fursa hiyo kutangaza bidhaa zao na kwamba, taratibu za kushiriki maonesho zianapatikana kwa kutembelea Ofisi ya SIDO Mkoa wa Shinyanga na Ofisi za Kanda.


PICHA ZA MITAMBO YA KUTENGENEZA MASHINE MBALIMBALI SIDO MKOA WA SHINYANGA

 




 


Post a Comment

0 Comments