Wakazi 22,482 wa Mji wa Misungwi na vijiji jirani wamenufaika na huduma bora zaidi ya majisafi, baada ya kukamilika kwa Mradi wa Upanuzi wa Mtandao wa Majisafi Misungwi Mjini wenye thamani ya Sh. milioni 888.
Mradi huo umeongeza upatikanaji wa maji kutoka asilimia 90 hadi 97, hatua inayolenga kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji na kuchochea shughuli za kijamii na kiuchumi.
Mradi umehusisha ujenzi wa kituo cha kusukuma maji, choteo lenye uwezo wa kuhifadhi lita 50,000, pamoja na matenki mawili yenye uwezo wa kuhifadhi lita 150,000 na 90,000. Pia, pampu mbili zenye uwezo wa kusukuma lita 50,000 kwa saa na transfoma yenye uwezo wa KV 100 zimefungwa.
Aidha, zimewekwa kilomita 3.5 za mabomba ya HDPE PN16 yenye ukubwa wa milimita 160 na 110, vituo 10 vya kuchotea maji na chemba 10 za valves.
Akizindua rasmi mradi huo leo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Mwang’onda, amesema mradi huo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu za kijamii, hususan maji safi na salama.
Mradi ulianza kutekelezwa Oktoba 2, 2023 na kukamilika Februari 9, 2026, na kwa sasa umeanza kutoa huduma kwa wananchi wa maeneo ya Ng’ombe, Iteja, Mbela B, Mbela D, Mbela C, Old Misungwi, Mwamanga na Mitindo B.
Mwang’onda amewataka wananchi kutunza miundombinu hiyo ili uwekezaji huo udumu na kuendelea kuwanufaisha wananchi kwa muda mrefu.
Kwa upande wao, wakazi wa maeneo hayo wameeleza kuwa mradi huo umepunguza changamoto ya kutafuta maji, huku vituo vya kuchotea maji vilivyo karibu na makazi vikiwasaidia wanawake na watoto kuokoa muda na kuutumia katika shughuli za uzalishaji na majukumu ya kifamilia.
Wakazi hao pia wamewataka wenzao kutunza miundombinu ya maji, wakisema upatikanaji wa maji kwa uhakika utasaidia kuboresha usafi wa mazingira na kuwawezesha wananchi kufanya shughuli zao za kiuchumi bila usumbufu.
Source IPP Media

0 Comments