WANAWAKE NA SAMIA-SHINYANGA WAJA NA SULUHISHO LA KUPUNGUZA GHARAMA ZA MKAA



Kikundi cha Wanawake na Samia-Shinyanga, kimewahimiza wakazi wa Shinyanga kutumia mkaa mbadala unaotokana na mabaki ya makaa ya mawe, unaosambazwa na kikundi hicho kwa bei chini ili  kulinda mazingira na kupunguza gharama za maisha kwa wananchi.

Akizungumza na SHINYANGA ONE MEDIA, Mwenyekiti wa kikundi hicho, Husna Mashaka Ally, amesema mkaa huo unapatikana kwenye Duka la Nishati Safi na Salama ya Kupikia wanalolimiliki, lililopo eneo la Bustani ya Kagunze, mtaa Mabambasi, Kata ya Ndembezi katika manispaa ya Shinyanga, ambalo lilizinduliwa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, Agosti 19, 2026.


Amesema mpaka sasa kikundi hicho kimepokea jumla ya tani tano za mkaa huo kutoka Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), unaouzwa kuanzia Shilingi Elfu moja kwa kilo, hatua inayolenga kuwawezesha wananchi wote, wakiwemo wenye kipato cha chini, kumudu gharama.

Kwa mujibu wa Husna, mkaa huo hautoi moshi, rafiki wa mazingira na ukiwashwa hudumu kwa saa tatu hadi nne, hivyo kumwezesha mtumiaji kupika chakula kingi kwa kutumia kiasi kidogo cha mkaa.

Husna amewaomba wananchi wa Shinyanga kukiunga mkono kikundi hicho kwa kununua na kutumia mkaa huo, hatua ambayo itachangia kuwainua wanawake kiuchumi na kusaidia  kupunguza uharibifu wa mazingira, unaotokana na ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa.

Akizungumzia mipango waliyonayo amesema, kikundi hicho kinajiandaa kutembelea shule, vyuo na taasisi nyingine zinazopika chakula kwa wingi, kwa lengo la kuhamasisha matumizi ya nishati hiyo ili kuongeza idadi ya watumiaji mkoani Shinyanga.

Wanawake na Samia ni kikundi cha wanawake kinachounga mkono ajenda za maendeleo za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ikiwemo juhudi za utunzaji wa mazingira, kwa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya RAFIKI BRIQUETTES

Post a Comment

0 Comments