WAZIRI MKUU ATAKA KAZI ZA UBUNIFU KUPELEKWA SOKONI BADALA YA KUKOMEA KWENYE MAONESHO

Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba ameitaka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na taasisi zake kuhakikisha bunifu zinazozalishwa na Watanzania haziishii kuonyeshwa kwenye maonesho, na badala yake ziendelezwe, kulindwa na kupelekwa sokoni ili ziwe suluhisho la changamoto mbalimbali zilizopo ikiwa ni pamoja na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa

Waziri Mkuu ametoa maelekezo hayo leo, Jumatatu, Agosti 24, 2026, jijini Tanga wakati akihitimisha Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu.

Waziri Mkuu ameitaja Tanzania kuwa ni nchi yenye wabunifu wenye uwezo mkubwa na kwamba, kinachotakiwa hivi sasa ni kuhakikisha ubunifu wao unapelekwa mbele zaidi kwa kuzalishwa kwa wingi na kuuzwa sokoni ili uweze kusaidia kuleta suluhisho la changamoto zilizopo, badala ya kukomea tu kwenye maonesho.

“Ni lazima tuvuke kwenye maonesho, twende kwenye uhalisia wa maisha kwamba hivi vitu ambavyo tunavionyesha kwenye maadhimisho kama haya sasa viende kwenye utaratibu wa kila siku wa maisha, tuvitengeneze vya kutosha, vitumike na viingie sokoni,” amesema Dkt. Mwigulu.

Kupitia kilele cha maonesho hayo, Dkt. Mwigulu ameahidi kuwa, Serikali itaendelea kuwekeza katika sayansi, ujuzi na ubunifu kwa lengo la kuyageuza maeneo hayo kuwa nguzo muhimu za uchumi wa Taifa na kuchochea maendeleo kupitia matumizi ya tafiti na teknolojia.

Wakati huohuo, amesema Serikali haitakubali kushusha viwango vya elimu, huku akisisitiza umuhimu wa taasisi zinazosimamia ubora wa elimu kuendelea kusimamia misingi ya kitaaluma katika kuandaa wataalamu wenye uwezo unaokubalika na kwamba, katika sekta nyeti kama afya, uhandisi na elimu, ubora wa mafunzo haupaswi kuchezewa.

Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amesema maonesho hayo yanathibitisha jitihada za Serikali katika kutekeleza maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuimarisha elimu inayounganisha nadharia na vitendo, ili kuandaa wahitimu wenye ujuzi wa kujiajiri na kuingia katika soko la ajira.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Caroline Nombo amesema jumla ya taasisi 91 za umma na binafsi zimeshiriki katika maadhimisho hayo, ambayo yamehusisha maonesho ya elimu, sayansi, teknolojia na ubunifu, mashindano ya kitaifa ya ujuzi na ubunifu pamoja na makongamano yaliyolenga kujadili mchango wa elimu, ujuzi na teknolojia katika kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Husna Sekiboko amesema Bunge litaendelea kuunga mkono jitihada za Serikali za kuendeleza elimu, ujuzi na ubunifu kupitia bajeti, sera na miongozo inayolenga kuwawezesha watafiti na wabunifu wa ndani kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa.

Amesisitiza umuhimu wa kuzipa kipaumbele bidhaa na teknolojia zinazozalishwa nchini, zikiwemo katika taasisi za Serikali, ili kuongeza matumizi ya bunifu za Watanzania na kuchochea ukuaji wa wabunifu hao.

 Kaulimbiu ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu mwaka 2026 ni “Elimu, Ujuzi na Ubunifu: Njia ya Kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

SOURCE: OFISI YA WAZIRI MKUU

Post a Comment

0 Comments