KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE ARIDHISHWA NA MIRADI YA MAENDELEO KATIKA MANISPAA YA SHINYANGA

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Mwang’onda, ameeleza kuridhishwa na namna ambavyo miradi ya maendeleo ilivyotekelezwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, hatua iliyomfanya  kuridhia kuizindua miradi hiyo.

Mwang’onda ameyasema hayo leo, Agosti 19, 2026, wakati akitembelea, kukagua, kuweka mawe ya msingi na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo, baada ya Mwenge wa Uhuru kuanza mbio zake katika Manispaa ya Shinyanga.

Awali, wakati akipokea Mwenge kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Peter Masindi, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro,  alisema Mwenge ukiwa katika Wilaya ya Shinyanga utatembelea jumla ya miradi 14 ya maendeleo.

Alifafanua zaidi kwamba, kati ya miradi hiyo, saba ipo katika Manispaa ya Shinyanga yenye thamani ya Sh. bilioni 5.2, huku mingine saba ikiwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga yenye thamani ya Sh. bilioni 5.4.

Mtatiro alibainisha kuwa, Fedha zote zilizotumika kutekeleza miradi hiyo zimeletwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, isipokuwa tu ile michache inayotokana na wawekezaji binafsi.

Ukiwa katika Manispaa ya Shinyanga, Mwenge wa Uhuru umekimbizwa umbali wa kilomita 84 na kufikia miradi mbalimbali, ikiwemo kuzindua mradi wa upanuzi wa mtandao wa maji katika Kata ya Kolandoto, uzinduzi wa Zahanati ya Kijiji cha Mwagala katika Kata ya Ibadakuli, pamoja na kuweka jiwe la msingi katika mradi wa mwekezaji binafsi wa Makindo Royal Hotel uliopo mjini Shinyanga.

Mwenge pia umekagua shughuli za Kikundi cha Vijana cha Mkasa Fashion kilichopo Shinyanga mjini, kuzindua duka la nishati safi ya kupikia la Kikundi cha Wanawake na Samia kilichopo katika Kata ya Ndembezi, kufungua Daraja la Dodoma linalowaunganisha wakazi wa Kata za Ngokolo na Ndembezi, kuzindua vyumba vinne vya madarasa katika Shule ya Sekondari Old Shinyanga pamoja na Klabu ya Wapinga rushwa katika Shule hiyo.

Shughuli za mbio za Mwenge wa Uhuru na uzinduzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Manispaa ya Shinyanga, zimehudhuriwa pia na Mbunge wa Jimbo la Shinyanga mjini ambaye pia ni waziri wa mambo ya ndani ya nchi, Paschal Patrobas Katambi.

Kesho Alhamisi, Mwenge wa Uhuru utakabidhiwa katika Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga (vijijini)
SOURCE: JAMII FOCUS

 

Post a Comment

0 Comments