FAHAMU UMUHIMU WA UWEPO WA MASOKO RASMI YA MADINI LIKIWEMO LA SHINYANGA

 

Wachimbaji wadogo wa madini, wakiwemo wa dhahabu na almasi, wameshauriwa kuuza madini yao kupitia masoko rasmi yaliyoanzishwa, ili kupata bei inayolingana na thamani halisi ya madini hayo.

Akizungumza na SHINYANGA ONE MEDIA, kuhusu umuhimu wa uwepo wa masoko rasmi ya madini kwenye mikoa na vituo vilivyoko kwenye maeneo ya uchimbaji, Msimamizi wa Soko Kuu la Madini Mkoa wa Kimadini Shinyanga, Mhandisi Gerad Kabeho, amesema masoko hayo yanawasaidia wachimbaji  kuuza madini yao kwa thamani inayostahili, huku Serikali ikihakikisha kodi na tozo zilizoelekezwa zinalipwa kwa kiwango kinachotakiwa.


Msimamizi wa Soko Kuu la Madini Mkoa wa Kimadini Shinyanga, Mhandisi Gerad Kabeho

Amesema kuuza madini kupitia masoko na vituo rasmi pia kunawasaidia wachimbaji wadogo na wachimbaji binafsi kuepuka kutapeliwa au kuuza kwa walanguzi, wanaoweza kutoa bei isiyolingana na thamani halisi ya madini.

Kwa mujibu wa Mhandisi Kabeho, madini yanapofikishwa kwenye masoko au vituo rasmi hupimwa na kuthaminishwa na wataalamu wa Serikali kwa kutumia vifaa vya kisasa, hatua inayosaidia kubaini thamani yake na kuwezesha muuzaji kupata bei inayostahili.

Mhandisi Kabeho amesema wanunuzi waliosajiliwa katika masoko na vituo hununua madini kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa, huku anayeuza akinufaika zaidi kupitia ushindani wa kibiashara unaozingatia bei elekezi inayotolewa na Serikali, kulingana na mwenendo wa bei katika soko la dunia.

Amesema mfumo huo unawapa wachimbaji wadogo nafasi ya kupata mapato na faida zaidi, tofauti na wanapouza madini yao kupitia njia zisizo rasmi ambazo ni kinyume cha sheria.

Akitoa mfano wa madini ya almasi, Mhandisi Kabeho amesema yanahitaji utaalamu wa hali ya juu ili kubaini thamani yake halisi, kwa kuwa kuyathaminisha madini hayo hutegemea vigezo mbalimbali, ikiwemo umbo lake, ubora, uzito na rangi.

Amesema wanunuzi wa mitaani hawazingatii vigezo hivyo na upimaji wa kitaalam, hatua ambayo inamweka mchimbaji katika hatari ya kupunjwa na Serikali kukosa mapato yake.

Mhandisi Kabeho ameyataja, madini yanayouzwa na kununuliwa katika mkoa wa kimadini Shinyanga kuwa ni pamoja na dhahabu, ambayo hupatikana kwa wingi, ikifuatiwa na almasi, pamoja na madini ya fedha yanayopatikana kwa kiasi kidogo kutoka nje ya mkoa.

Mkoa wa Kimadini Shinyanga, kwa sasa una jumla ya wanunuzi wakubwa wa madini 25, ambao shughuli zao zinasimamiwa na Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa, kwa niaba ya Tume ya Madini iliyo chini ya Wizara ya Madini.

Aidha, vituo vya wanunuzi wadogo wa madini vilivyopo kwenye maeneo ya uchimbaji kwa upande wa dhahabu ni Mwakitolyo, Nyandolwa na Mwanubi ambavyo vyote viko katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga na Itilima-mwazezema kilichopo  wilayani Kishapu. 

Vituo vinavyonunua madini aina ya Almasi ni viwili ambavyo ni Maganzo kilichopo katika wilaya ya Kishapu na Jimondoli-Ng'wampangabule kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.

Kulingana na sheria na miongozo inayosimamia biashara ya madini, wachimbaji wadogo hawaruhusiwi kuuza moja kwa moja madini yao nje ya nchi na badala yake wanauza kwa  wanunuzi wadogo (Brokers) kupitia vituo vilivyoko kwenye maeneo ya uchimbaji  au kwa wanunuzi wakubwa (Dealers) kupitia soko kuu la madini kwenye mkoa. 

Kwa upande wa wachimbaji wenye leseni za uchimbaji wa kati (ML) na leseni maalum za uchimbaji wa madini wanazopewa wachimbaji wakubwa (SML) wao wanaruhusiwa kuuza madini waliyoyazalisha kupitia soko lolote watakalolichagua ikiwemo nje ya nchi.

Masoko rasmi ya madini nchini, yalianzishwa na Serikali kufuatia marekebisho ya Sheria ya Madini ya mwaka 2017, kupitia Kifungu cha 27C cha Sheria ya Madini, Sura ya 123 kikisomwa pamoja na kanuni zake za mwaka 2018.

Kifungu hicho cha sheria, kilianzisha mfumo wa masoko rasmi ya madini na kuipa Tume ya Madini mamlaka ya kuanzisha masoko hayo, ambapo pamoja na mambo mengine, kinatoa sharti kwa watu wanaotaka kuuza au kununua madini kufanya hivyo kupitia masoko rasmi ya madini.

Masoko hayo ya madini, yalianza kufanya kazi rasmi Machi 2019, yakiwa na lengo la kudhibiti utoroshaji na biashara haramu ya madini, kuhakikisha Serikali inakusanya kodi na tozo zinazotakiwa kwa ukamilifu, pamoja na kuwawezesha wachimbaji wadogo kuuza madini yao kupitia mfumo rasmi na kwa bei inayolingana na thamani halisi.

Post a Comment

0 Comments