JAJI WARIOBA AISHIWA NGUVU NA KUDONDOKA WAKATI AKIHUTUBIA MKUTANO WA TCD

 

Makamu wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Sinde Warioba, amedondoka ghafla wakati akihutubia Mkutano wa Kitaifa wa kujadili hali ya kisiasa nchini, Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 na mustakabali wa Taifa unaofanyika jijini Dar es Salaam.

Jaji Warioba alikuwa akizungumza katika mkutano huo ulioandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), ambapo alikuwa ni mgeni rasmi.

Tukio hilo limetokea wakati Jaji Warioba akieleza hoja mbalimbali kuhusu hali ya kisiasa nchini, huku akisisitiza masuala yanayohusu mustakabali wa taifa na umuhimu wa kujenga mazingira yanayolinda demokrasia.

Baada ya kuanguka, watu waliokuwa karibu naye walimsaidia na kumtoa ukumbini kwa ajili ya kupatiwa msaada.

Hata hivy, Mwenyekiti wa TCD, Dorothy Semu, amewaambia washiriki wa mktanao huo kwamba, hali ya Jaji Warioba imetengamaa na amekwenda kupumzika.

Mkutano huo umehudhuriwa na vyama vya siasa kikiwemo Chama Cha Mapinduzi (CCM), Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa Tanzania, Juma Ali Khatib, makundi ya uwakilishi wa vijana, wafanyabiashara pamoja na mabalozi kutoka nchi mbalimbali.

Akizungumza kabla ya kukutwa na hali hiyo, Jaji Warioba, ameshauri misingi ya usawa, uadilifu, uwajibikaji na uzalendo, iimarishwe ikiwa ni njia ya kujenga amani ya kudumu.

Amesema vyama vya siasa vina wajibu wa kuhakikisha ushindani wa kisiasa haugeuki kuwa chanzo cha kuwagawa Watanzania.

Kwa upande wake,Msajili wa vyama vya siasa nchini Jaji Francis Mtungi amesema ushiriki wa wadau hao unaonyesha dhamira ya kutafuta muafaka kwa maslahi mapana ya taifa.

Balozi wa Ireland nchini, Nicola Brennan, amesema uzoefu wa nchi mbalimbali unaonesha kuwa imani inaweza kujengwa upya na taasisi za kidemokrasia kuimarishwa kupitia mazungumzo na mageuzi.

Balozi wa Uswisi nchini, Nicole Providoli, yeye amesisitiza mshikamano wa kitaifa kwamba unajengwa pale mitazamo tofauti ndani ya jamii inaposikilizwa na kuzingatiwa.

 

Post a Comment

0 Comments