Akizungumza na SHINYANGA ONE MEDIA, Meneja Miradi wa
RAFIKI SDO, George Nyamboto, amesema shirika hilo limetekeleza miradi
mbalimbali ya kutetea haki za watoto katika mkoa wa Shinyanga, hatua ambayo
imewasaidia watoto kufahamu, kudai na kutetea haki zao.
Amesema mafanikio ya kazi wanazozifanya yamewezesha watoto wawili kutoka mkoa wa
Shinyanga kuchaguliwa kuongoza baraza la watoto ngazi ya taifa kwa awamu mbili
mfululizo, ambao ni Nancy Aloyce Kasembo aliyeongonza baraza hilo kuanzia
mwaka 2021 hadi 2023, akifuatiwa na Raphael Charles Joseph aliyeongoza baraza hilo kuanzia mwaka 2023 hadi 2025.
Nyamboto amebainisha kuwa, kupitia madawati hayo waliyoanzisha katika shule za msingi na sekondari, watoto hukutana na kujadili
changamoto mbalimbali zinazokwamisha ustawi na maendeleo yao, katika mazingira ya nyumbani na
shuleni.
Amesema kwa vile watoto wana uelewa wa kutosha kuhusu haki
zao, huwasilisha changamoto wanazoziona kwa walimu na ngazi nyingine za maamuzi
kwa ajili ya kushughulikiwa, jambo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa
kuboresha mazingira ya kujifunzia na kupunguza vitendo vya ukatili kwa watoto.
Akizungumzia mradi wa MKUA ambao wanaendelea kuutekeleza kwenye Halmashauri zote sita za mkoa wa
Shinyanga, amesema kupitia mradi huo wa miaka sita ulioanza
mwaka 2022, kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo na Ushirikiano wa Kimataifa
la Sweden (SIDA), RAFIKI SDO imefanikiwa kuanzisha madawati ya ulinzi na
usalama wa mtoto katika shule 36 za msingi na Sekondari zinazonufaika na
mradi huo.
Kwa mujibu wa Nyamboto, kupitia mradi huo pia wameweza
kuzishawishi shule kutumia mapato yake kununua taulo za kike kwa ajili ya
wanafunzi wa kike wanapokuwa katika kipindi cha hedhi, hatua ambayo imewaongezea
kujiamini na kupata motisha ya kusoma.
Vilevile wamewajengea uwezo walimu ili waweze kuwasaidia watoto wenye
ulemavu kulingana na mahitaji yao pamoja na kushawishi vyombo vya
maamuzi kuongeza bajeti kwa ajili ya masuala yanayohusu watoto.
Aidha, RAFIKI SDO imekuwa ikiwajengea uwezo viongozi wa shule ili washirikiane na wazazi katika kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula shuleni, hatua ambayo imewapa watoto hamasa kupenda kusoma na kupunguza hali ya utoro.
Nyamboto pia ameeleza kuhusu mradi wa MWALIMU KWANZA,
ELIMU BORA unaotekelezwa na RAFIKI SDO katika Wilaya ya Bukombe mkoani Geita,
ambao ameutaja kuwa unalenga kutoa motisha kwa walimu na kuboresha mazingira ya
ufundishaji .
Kupitia mradi huo unaofadhiliwa na Mtandao wa Elimu
Tanzania (TEN/MET) ulioanza kutekelezwa kuanzia Julai, 2026, hadi Juni 2028,
wanaboresha mazingira ya ufundishaji na kuwajengea walimu uwezo kupitia mafunzo
mbalimbali, ikiwemo matumizi ya TEHAMA katika ufundishaji.
Pia, RAFIKI SDO inatoa elimu kwa jamii kupitia mikutano ya
hadhara kuhusu umuhimu wa kuthamini mchango wa walimu, ili waweze kushirikiana
nao katika kuhakikisha watoto wao wanapata elimu bora.
Aidha, wanafadhili uanzishwaji wa vituo viwili vya walimu katika Kata za Bulangwa na Uyovu, kwa ajili ya kuwawezesha walimu kujiendeleza kitaaluma.
0 Comments